MTOTO MWENYE ULEMAVU ABAKWA NA KUPATA UJAUZITO BUNGI

Na Abdul Sakaza.

Akiripoti Kutoka Bungi, Wilaya Ya Kati Unguja.

Wananchi wa Shehia ya Bungi, Wilaya ya Kati Unguja, wameitaka serikali kuharakisha hatua za kisheria dhidi ya mtuhumiwa wa ubakaji wa mtoto mwenye ulemavu wa viungo, wakihofia huenda haki ya mtoto huyo ikadidimizwa.

Wakizungumza na WaandishiwaHabari, wakazi wa eneo hilo walisema tukio hilo limewaumiza na kuibua hisia kali kutokana na hali ya mtoto huyo ambaye hana uwezo wa kujitetea.

Mama mzazi wa mtoto huyo alieleza kuwa hakugundua mapema kuhusu ujauzito wa binti yake hadi alipigiwa simu na walimu wa skuli wakimtaarifu kuwa mtoto wake ameanguka na anahitaji kufikishwa hospitalini.

“Nilipofika skuli nilimkuta mwanangu akiwa ofisini na walimu wake, wakaniambia nimpeleke hospitali ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (ZU) kwa uchunguzi. Nilipofika huko ndipo madaktari waliponiambia ana ujauzito,” alisema kwa huzuni.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, alimhoji mwanawe kuhusu aliyempa ujauzito na ndipo mtoto akamtaja kijana anayefahamika kwa jina la Buruhani, ambaye alikuwa akimfuata nyumbani kila wakati mama yake anapokuwa hayupo na Baada ya maelezo hayo, mama huyo aliripoti tukio hilo kwa uongozi wa skuli na Sheha wa Shehia ya Bungi.

Baada ya kupewa fomu ya uchunguzi wa afya, mama huyo alimpeleka mtoto hospitali ya Mwera–Pongwe, ambapo madaktari walithibitisha kuwa ana ujauzito wa miezi minne na Mtoto huyo, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema siku aliyofanyiwa kitendo hicho mtuhumiwa alimkuta nje ya nyumba yao, kisha akamvuta hadi ndani ya boma la nyuma lililokuwa karibu na kumfanyia kitendo hicho.

Hata hivyo, mama wa mtoto huyo alielezwa kuwa kesi hiyo italazimika kufuata taratibu za kisheria kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi na ameombwa kua mstahamilivu kupitia kesi hiyo huku taratibu za awali zikichukuliwa

Siku chache baadaye, mratibu wa shehia hiyo bii alimchukua mama huyo na kwenda naye kituo cha polisi Tunguu kutoa maelezo rasmi ambapo Polisi wa kituo hicho walimjulisha kuwa mamlaka ya kesi hiyo ipo chini ya kituo cha polisi Unguja Ukuu, ambako baadaye jalada la kesi lilihamishiwa.

Sheha wa Shehia ya Bungi, Vuai Ramadhan Vuai, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa uchunguzi wa polisi unaendelea huku mtuhumiwa akiwa mikononi mwa vyombo vya usalama.

“Tumepewa taarifa rasmi na tayari polisi wanaendelea na hatua za uchunguzi. Tunawaomba wazazi wawe karibu zaidi na watoto wao, na vijana waache tabia za udhalilishaji,” alisema Sheha.

Kwa upande wake, mwanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia, Sabah Bakar Hassan, alisema matukio kama hayo bado yanaendelea licha ya juhudi za kutoa elimu kwa jamii.

“Kwa sasa tunafuatilia tukio hili la mtoto mwenye mahitaji maalum aliyebakwa na kupewa ujauzito na mtu anayedaiwa kuwa na umri wa miaka 30. Tunasisitiza jamii kuendelea kupata elimu juu ya haki za watoto na madhara ya ukatili wa kijinsia,” alisema.

Mwanaharakati huyo aliongeza kuwa ushirikiano kati ya wazazi, viongozi wa shehia na vyombo vya sheria ni muhimu kuhakikisha waathirika wanapata haki zao ipasavyo na wahalifu wanachukuliwa hatua stahiki.

Kwa sasa, mtuhumiwa anashikiliwa na jeshi la polisi katika kituo cha Unguja Ukuu, akisubiri taratibu zaidi za kisheria.

One thought on “MTOTO MWENYE ULEMAVU ABAKWA NA KUPATA UJAUZITO BUNGI

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *