MTO WA PWANI YAONGOZA UKATAJI WA MIKOKO KASKAZINI UNGUJA

Na Abdul Sakaza

Akiripoti Kutoka Kaskazini Unguja

Sakaza Digital Climatic Change/ Follo Up Story

Shehia Ya Mto Wa Pwani imetajwa kuongoza kwa ukataji na uharibifu wa Mikoko Mkoa Wa Kaskazini Unguja, ikifuatiwa na Tumbatu, huku Muwanda ikishika nafasi ya tatu.

Kwa upande mwingine, Shehia ya Kiongwe Kidogo imetajwa kuwa kinara wa uhifadhi wa Mikoko kwa kutokata misitu hiyo na kuwa mfano wa kuigwa katika juhudi za uhifadhi wa Mazingira ya Pwani Mkoani humo.

Taarifa hiyo imetolewa na Afisa Misitu Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Sleyum Saidi Khamis, wakati akizungumza na mwandishi wa habari wa Sakaza Digital mapema wiki hii ambapo amesema kwa mwaka 2025 jumla ya mikoko 5,050 imekatwa katika shehia za Mto wa Pwani, Tumbatu na Muawada.

Kulingana na taarifa hiyo, Mto wa Pwani inaongoza kwa kukatwa mikoko 2,900, ikifuatiwa na Tumbatu mikoko 1,200, huku Muwanda ikirekodi mikoko 950 iliyokatwa.

Amesema licha ya kiwango hicho cha uharibifu, Serikali kwa kushirikiana na vikundi vya uhifadhi na wadau wa mazingira imefanikiwa kupanda jumla ya mikoko elfu nane(8,000) katika shehia za Tumbatu, Muwanda, Bumbwini, Kiongwe Kidogo, Fujoni na Mto wa Pwani, kama sehemu ya mkakati wa kufidia mikoko iliyoharibiwa na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Afisa huyo pia  amesema ingawa juhudi za upandaji wa mikoko zinaendelea, bado changamoto ya ukataji wa mikoko kwa ajili ya kuni na ujenzi inaendelea kujitokeza katika baadhi ya maeneo hali inayohitaji ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na jamii.

Kunaathari Gani Kukata Mikoko Kisiwani Tumbatu?

Dokta Sharif Alawi Badru ni Mtaalamu wa Mazingira na Majanga ya Asili kutoka Mombasa Nchini Kenya ameweka bayana kua kukata mikoko katika maeneo ya visiwa kama vile Tumbatu kunaweza kusababisha kutokea majanga asilia kama vile upepo mkali wenye madhara  ,kupanda kwa kina cha maji ya Bahari katika makaazi ya watu na mmong’onyoko wa aridhi.

“Kukata mikoko Tumbatu ni hatari sana. Upepo unapovuma unaingia moja kwa moja katika makazi ya watu, na ndiyo maana Tumbatu imekuwa ikiathiriwa mara kwa mara, kwa sababu mikoko ambayo ni kizuizi cha asili cha upepo inaendelea kukatwa,” aliesema.

Ameongeza kuwa mikoko ni ngao muhimu dhidi ya mmomonyoko wa ardhi na mawimbi makali ya bahari, hivyo kuendelea kuharibiwa kunahatarisha makazi, mashamba na miundombinu ya kijamii ya wakazi wa kisiwa hicho.

Aidha, ukataji wa mikoko Tumbatu unasababisha kupungua kwa mazalia ya samaki, hali inayowaathiri moja kwa moja wavuvi na wananchi wanaotegemea bahari kwa kipato na chakula, jambo linaloathiri ustawi wa uchumi wa jamii hiyo

Kwa Nini Mikoko  Mto wa Pwani Inakatwa

Mbarouk Khamis Zahor ni  Mwenyekiti wa Kikundi cha Hifadhi ya Bahari Mto wa Pwani, Akizungumzia suala la ukataji wa mikoko katika Shehia hiyo  amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo licha ya jitihada za uhifadhi na upandaji wa mikoko   zinazofanywa na kikundi chao.

“Ni kweli changamoto bado ipo. Licha ya jitihada zetu, zaidi ya mikoko 2,900 imekatwa Mto wa Pwani,” amesema Mbarouk.

Amesema mikoko hiyo hukatwa zaidi na wananchi kutoka maeneo jirani ya Mkokotoni na maeneo mengine  kwa ajili ya shughuli za ujenzi na matumizi ya kuni, hali inayochangia kuendelea kwa uharibifu wa misitu hiyo muhimu ya pwani.

Mbarouk amesema kwa sasa kikundi cha hifadhi ya Bahari , kwa kushirikiana na viongozi wa shehia, kimeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha hakuna nyumba wala vibanda vinavyojengwa kwa kutumia mti wa  mikoko.

“Tumeamua kusimamia kwa ukali matumizi ya mikoko ili kuzuia uharibifu zaidi,” ameongeza.

Amesema juhudi hizo zinaambatana na utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa mikoko katika kulinda fukwe dhidi ya mmomonyoko wa ardhi, kuhifadhi mazalia ya viumbe wa baharini na kuimarisha maisha ya wananchi wanaotegemea uvuvi.

Wanawake Wa Mto Wapwani Wanaathirika Vip Na Ukataji Wa Mikoko

Bii Mwanaidi Hamad (60), mkazi wa Mto wa Pwani ni  Katibu wa Kikundi cha Hifadhi ya Bahari, amesema ukataji wa mikoko unaathiri kwa kiwango kikubwa maisha ya wanawake wa eneo hilo kwani kupitia kikundi hicho huweka makusanyo ya fedha ambayo huwasadia kukopeshana ili kukidhi mahitaji yao ya kimaisha.

“Mikoko ni chanzo cha maisha yetu. Unapokata mikoko unawaathiri wanawake moja kwa moja na unarejesha nyuma juhudi zetu za kujikimu kimaisha,” amesema.

Kando na hilo Semeni Dadi Haji ni mjumbe wa kikundi hicho amewaomba wanaojihusisha na suala la ukataji wa Mikoko katika Shehia Ya Mto Wa Pwani  kuacha maramoja ili kutimiza ndoto za wanawake za kujikwamua na umasikini kupitia mikoko na wamewaomba wahisani kuwapatia vitendea kazi vinavyohitajika  ili kuendelea kuhifadhi na upandaji wa Mikoko.

Kwa upande wake, Sheha wa Shehia ya Mto wa Pwani, Moh’d Ali Ali, amesema uongozi wa shehia unatambua juhudi za kikundi cha hifadhi ya Bahari  na umekuwa ukishirikiana nao katika kila hatua ya kupanda, kutunza na kuhifadhi mikoko, kama mkakati wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Pia amepongeza juhudi za wananchi wa Kiongwe Kidogo kwa kuonyesha uelewa na uzingatiaji wa sheria za uhifadhi wa mazingira huku akitumia mfano huo  kuwataka wananchi wa shehia yake kuiga mfano huo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *