NA FAUZIA MUSSA
KATIBU Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Abeda Rashid Abdallah, amesema malezi na makuzi ya awali ya mtoto ni nguzo muhimu ya maendeleo ya taifa lolote, hivyo ni lazima familia kuwekeza ipasavyo katika miaka ya mwanzo ya maisha ya mtoto.
Akifungua kikao kazi kilichofanyika katika hoteli ya Visitors Inn, Jambiani, mkoa wa Kusini Unguja, kuhusu Mradi wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (ECCD), alieleza kuwa kufanya hivyo kunapunguza changamoto za kiafya, kijamii na kielimu zinazoweza kujitokeza baadae.
Alisisitiza kuwa ushirikiano baina ya jamii, familia na taasisi zinazohusika na ulinzi, makuzi na matunzo ya watoto n i muhimuili kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na makuzi stahiki.“Tunataka kuona kila mzazi, mlezi na mtoa huduma anakuwa na maarifa sahihi ya kulea mtoto kwa upendo, ulinzi na kwenye mazingira bora ya kujifunzia”, alisema Katibu Abeda.
Aidha, alitoa wito kwa watekelezaji wa programu hiyo kushirikisha jamii kupitia vikundi vya wanawake, wazazi, taasisi za dini na mifumo ya kijamii ili kuharakisha kufikisha ujumbe wa malezi chanya na kukumbushia umuhimu wa kujumuishwa kwa watoto wenye ulemavu na ushiriki wa wanaume katika malezi ya awali ya watoto kwani ni miongoni mwa changamoto zinazokwaza makuzi bora ya watoto.
Kwa upande wake, Mratibu wa wa mradi wa ECCD Zanzibar, Dk. Maryam Issa Juma, alisema kikao hicho kinapania kuimarisha utekelezaji wa programu ya malezi bora, lishe, afya, elimu ya awali na ulinzi wa mtoto.
Aliongeza kuwa mradi huo unalenga kufikia watoto 276,000 ifikapo mwaka 2030, hususani wenye umri wa miaka 0 hadi 8, sambamba na utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto.
Nae Naibu Katibu Mkuu Taaluma, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Dk. Mwanaisha Khamis Ameir, alibainisha kuwa malezi bora ya awali yanachangia mafanikio ya kitaaluma na wizara imeanzisha programu ya ‘Early Childhood Education’ pamoja na kujenga skuli za maandalizi zenye mazingira rafiki.
kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya, Fatma Kabole, alisisitiza umuhimu wa huduma za afya kwa mama na mtoto, chanjo na lishe bora, huku Ofisa Mipango kutoka Wizara ya Kilimo, Hamad Massoud Ali, akihimiza familia kuanzisha bustani za nyumbani ili kuongeza upatikanaji wa mboga na matunda.Mtaalamu wa Hifadhi ya Mtoto kutoka UNICEF, Ahmed Rashid Ali, alisema asilimia 18 ya watoto Zanzibar wanakabiliwa na udumavu na asilimia 40 wanakosa makuzi stahiki kutokana na upungufu wa huduma bora za awali.“Mtoto anahitaji kuhifadhiwa dhidi ya msongo wa mawazo hasa katika siku 100 za mwanzo wa maisha yake kwani ni muhimu sana kwa ukuaji na maisha yake ya baadae”, alieleza Ahmed.
Mwezeshaji na mtaalamu wa masuala ya ECD, Mwalim Sharifa Suleiman alieleza watoto wanaopata malezi yenye muitikio chanya hupata mafanikio zaidi katika maisha yao.
Mkutano huo wa siku tatu ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa na sekta za elimu, ustawi wa jamii, afya na kilimo unasimamiwa na Taasisi ya Rais Ufuatiliaji Utendaji serikalini (ZPDB) umehudhhuiwa na taasisi za serikali, mashirika binafsi na Asasi za Kiraia ikiwemo Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), SOS, Milele Zanzibar Foundation, Mwanamke Initiative Foundation (MIF) na Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZBMF).
