KWANINI ZRA IMEVUKA LENGO LA MAKUSANYO YA KODI DISEMBA,WANANCHI WATIA NENO

Na Abdul Sakaza
Akiripoti kutoka Zanzibar
imeboreshwa saa 9 zilizopita

Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imetangaza kufanikiwa kuvuka lengo la makusanyo ya kodi kwa mwezi wa Disemba 2025 baada ya kukusanya Shilingi bilioni 90.873 sawa na ufanisi wa asilimia 100.39 ya makisio ya Shilingi bilioni 90.524.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya ZRA iliyotolewa Januari 02, 2026, makusanyo hayo yanaonyesha ongezeko kubwa ikilinganishwa na makusanyo ya mwezi huo huo wa mwaka wa fedha uliopita wa 2024/2025, ambapo ZRA ilikusanya Shilingi bilioni 75.583, hali inayothibitisha ukuaji wa makusanyo kwa asilimia 20.23.

Ukuaji wa Mapato Waendelea Kuimarika

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha mazingira ya biashara na usimamizi wa mapato zinaendelea kuzaa matunda, hususan katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Oktoba–Disemba).

Katika kipindi hicho, ZRA ilikadiriwa kukusanya Shilingi bilioni 286.813, lakini ilifanikiwa kukusanya Shilingi bilioni 273.772, sawa na ufanisi wa asilimia 95.45. Makusanyo hayo ni ongezeko la Shilingi bilioni 45.67 ikilinganishwa na robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo Shilingi bilioni 228.098 zilikusanywa.

Oktoba na Novemba kwanini Zikiweka Msingi

Takwimu zinaonesha kuwa katika mwezi wa Oktoba 2025, ZRA ilikusanya Shilingi bilioni 91.608 kati ya makisio ya Shilingi bilioni 101.266, huku Novemba ikishuhudia makusanyo ya Shilingi bilioni 91.291 dhidi ya makisio ya Shilingi bilioni 95.024. Hali hiyo ilichangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya makusanyo ya Disemba na robo nzima ya pili.

ZRA imeeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na sababu kadhaa ikiwemo kuimarika kwa shughuli za kiuchumi kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, hali inayochangiwa na sera na uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, zilizoimarisha mazingira ya biashara ndani ya Muungano.


Aidha, uwekezaji mkubwa katika miradi ya miundombinu na huduma za kijamii Zanzibar, chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, umetajwa kuwa kichocheo kikubwa cha ongezeko la shughuli za kiuchumi na ulipaji wa kodi.

Sababu nyingine ni kuongezeka kwa uelewa wa walipakodi kutokana na elimu inayotolewa na ZRA, kuimarika kwa ulipaji wa kodi kwa hiari, pamoja na utekelezaji wa msamaha wa adhabu na riba kwa walipakodi wenye madeni ya muda mrefu (Tax Amnesty).

Kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Januari–Machi), ZRA imetangaza kuendelea kuimarisha mikakati ya ukusanyaji wa mapato ikiwemo kuhakikisha mifumo yote ya kibiashara ya walipakodi inaunganishwa na Mfumo wa Kielektroniki wa Kutolea Risiti (VFMS).

Mamlaka hiyo pia itaendelea kusogeza huduma za kodi karibu na walipakodi kupitia kambi za kodi katika maeneo ya biashara, kufanya kampeni za uhamasishaji wa ulipaji kodi wa hiari, pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa miradi yote ya Serikali inayotekelezwa ili kukusanya kodi stahiki.

Wito kwa Walipakodi

Akizungumza kupitia taarifa hiyo, Mkuu wa Kitengo cha Habari, Uhusiano na Huduma kwa Walipakodi ZRA, Makame Khamis Mohd, amewashukuru walipakodi wote kwa ushirikiano wao na kuwataka kuendelea kulipa kodi kwa hiari ili kuiwezesha Serikali kuimarisha huduma za kijamii na maendeleo ya wananchi “Makusanyo haya ni matokeo ya ushirikiano mzuri baina ya ZRA, walipakodi na taasisi nyingine za Serikali. Tunaomba ushirikiano huo uendelee katika mwaka 2026,” amesema Makame.

ZRA imesisitiza kuwa mapato hayo ni nguzo muhimu ya maendeleo ya Zanzibar na kuwatakia walipakodi wote mafanikio na baraka za mwaka mpya wa 2026.

Wananchi Wa Zanzibar Waipongeza ZRA

Baadhi ya wananchi wa Zanzibar wameipongeza Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) kwa kuvuka lengo la makusanyo ya kodi kwa mwezi wa Disemba 2025, wakisema mafanikio hayo yanaonesha uwajibikaji, usimamizi mzuri wa mapato na mwelekeo chanya wa uchumi wa Zanzibar.

Mkazi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Salma Juma, amesema kuwa kuvuka lengo la makusanyo ni ishara kwamba juhudi za Serikali na ZRA katika kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari zimeanza kuleta matokeo chanya. “Tunapoona kodi zetu zinakusanywa vizuri, tunapata imani kuwa zitarejeshwa kwenye huduma za jamii kama afya, elimu na miundombinu,” amesema.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa soko la Darajani, Haji Bakari, amesema maboresho ya mifumo ya kodi na elimu inayotolewa na ZRA yamepunguza usumbufu kwa walipakodi na kuongeza uwazi. “Kwa sasa mifumo ni rahisi na huduma zimesogezwa karibu, jambo linalotupa motisha ya kulipa kodi kwa hiari,” amesema.

Nao vijana wameeleza kuwa mafanikio ya ZRA yanatoa matumaini ya kuimarika kwa uchumi na fursa za ajira. Mkazi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Juma Ali, amesema kuwa “mapato yanapokusanywa ipasavyo, Serikali inakuwa na uwezo wa kuwekeza zaidi kwenye miradi ya maendeleo itakayowanufaisha wananchi, hususan vijana.”

Wananchi hao wameitaka ZRA kuendeleza juhudi zake za kutoa elimu kwa walipakodi, kuimarisha mifumo ya kielektroniki na kudumisha uwazi ili kuongeza imani ya wananchi na kuendeleza mwenendo chanya wa makusanyo ya kodi Zanzibar.

              “Tulipe Kodi kwa Maendeleo ya Zanzibar”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *