KWANINI TUMBATU YAONA TUMAINI JIPYA LA AFYA

Na Abdulkadir Sakaza

Follow-Up Story

Imeboreshwa Saa 9 Zilizopita

Wananchi wa Kisiwa cha Tumbatu wamepokea kwa matumaini makubwa uwekaji wa Jiwe la Msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Tumbatu, wakisema mradi huo ni hatua muhimu katika kumaliza changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa huduma za afya, hasa kwa wanawake wajawazito, watoto, wazee na wagonjwa wa dharura.

Kwa miaka mingi, wakazi wa kisiwa hicho wamekuwa wakilazimika kuvuka bahari kufuata huduma za afya katika vituo vilivyopo nje ya Tumbatu. Safari hizo, kwa mujibu wa wananchi, zimekuwa hatarishi, zenye gharama kubwa na mara nyingi zimesababisha kuchelewa kwa matibabu, hali iliyochangia madhara makubwa kiafya na wakati mwingine kupoteza maisha.

Changamoto Za Afya Zilizopo Sasa Kisiwani Tumbatu

Wakazi wa Tumbatu wamesema ukosefu wa kituo cha afya chenye uwezo wa kutoa huduma za uhakika kwa saa 24 uliwalazimu wengi wao kutafuta matibabu nje ya kisiwa, hata kwa magonjwa ya kawaida. Changamoto hiyo imekuwa kubwa zaidi kwa wagonjwa wa dharura na wanawake wanaojifungua nyakati za usiku.

Asha Ali Makame (45), mkazi wa Tumbatu Uvivini na mama wa watoto saba, amesema wanawake wengi wa Tumbatu wamekuwa wakiishi katika hofu kubwa wakati wa kujifungua kutokana na kutokuwepo kwa huduma za dharura pia baadhi yao huamua kuondoka Kwenda nje ya kisiwa kwa familizia zao zinazoishi huko ili kujiweka karibu vituo vya afya vinavyotoa huduma za dharura .

“Nilipoteza mwanangu kwa sababu nilipofika kituo cha afya usiku hakukuwa na daktari wala huduma za haraka. Tukio hilo limeacha maumivu makubwa, lakini leo uwekaji wa Jiwe la Msingi la kituo hiki umetupa matumaini mapya,” amesema Asha kwa huzuni.

Wananchi Waeleza Imani Iliyopotea

Baadhi ya wakazi wamesema licha ya kuwepo kwa kituo cha afya cha awali kisiwani tumbatu , ukosefu wa vifaa tiba, wataalamu na dawa uliwafanya wengi kukosa imani na huduma zilizokuwepo.

Juma Haji Makame, mkazi wa Tumbatu jongowe , amesema wananchi wengi walikuwa wakihisi baadhi ya magonjwa hayawezi kutibiwa kisiwani kutokana na udhaifu wa miundombinu ya afya “Kulikuwa na hofu kubwa. Watu waliona ni bora kuvuka bahari kutafuta matibabu, hata kama ni hatari. Sasa ujenzi wa kituo hiki umeturejeshea imani kwa Serikali,” amesema Juma Haji Makame .

Kwa upande wake, Kazija Ali Makame  mkazi wa Tumbatu gomani , amesema wanawake wengi walikuwa wakilazimika kushawishika kusafiri hata wakiwa wagonjwa au wajawazito kwa sababu ya kutokuwa na uhakika wa huduma kisiwani humo.

“Tulikuwa tunaambiwa kuna kituo cha afya, lakini ukifika hukuti dawa wala mtaalamu. Ilitulazimu kwenda ng’ambo hata kama hali ya mgonjwa siyo nzuri,” alisema Kazija.

Mume wa bii kazija anaetambulika kwa jina la Sheha  Haji Makame, amesema hali hiyo iliongeza mzigo wa kifamilia na kiuchumi, hasa pale familia ilipolazimika kugharamia safari na matibabu kwa wakati mmoja.

“Mbali na hatari za safari, gharama zilikuwa kubwa. Mara nyingi tulikopa kuuza chochote  ili kumpeleka mgonjwa nje ya kisiwa. Ndiyo maana mradi huu ni faraja kubwa kwetu,” alisema Sheha .

Vijana Waona Zaidi ya Huduma za Afya

Kwa upande wa vijana, mradi huo umeonekana pia kama fursa ya kiuchumi. Haji Sheha Haji (19) amesema ujenzi wa Kituo cha Afya Tumbatu umeamsha matumaini mapya miongoni mwa vijana wa kisiwani.

“Tunatarajia si huduma za afya pekee, bali pia ajira kwa vijana wazawa wenye sifa. Tumechoka kuona wataalamu wote wakitoka nje wakati sisi tuna uwezo,” alisema.

Kwa upande wake, Amina hassan Omar (23), mkazi wa Tumbatu Jongowe, amesema wanawake vijana wanauona mradi huo kama fursa ya kujengewa uwezo na kushiriki moja kwa moja katika utoaji wa huduma za afya na kazi zinazohusiana na uendeshaji wa kituo hicho.

“Tunatarajia Serikali itatupa nafasi ya mafunzo na ajira, hasa sisi wasichana na wanawake vijana, ili nasi tushiriki katika kuwahudumia wananchi wetu,” alisesema Amina.

Haji adam haji (25), amesema ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana wa kisiwani na kuchochea uchumi wa familia.“Ajira zitakazopatikana hapa zitasaidia familia nyingi kujitegemea. Tunaomba Serikali itekeleze ahadi ya kuwapa kipaumbele vijana wazawa wenye sifa,” alisema Haji.

Wazee kisiwani wamesema changamoto za umri zilifanya safari za baharini kutafuta matibabu kuwa mateso makubwa kwao. Hata hivyo, wameeleza kuwa uamuzi wa Serikali kujenga kituo hicho, licha ya kuchelewa, umefika wakati muafaka.“Kwa wazee, kusafiri baharini ni mateso makubwa. Mara nyingi tulikaa kimya tukisubiri. Leo tunaona Serikali imetusikia,” alisema Mzee Makame Makame Haji.

Tahadhari ya Wananchi Kuhusu Uendeshaji

Pamoja na matumaini hayo, baadhi ya wananchi wameonya kuwa mafanikio ya mradi huo hayatategemea ujenzi wa majengo pekee, bali pia upatikanaji wa wataalamu, dawa, vifaa tiba na uendeshaji endelevu wa kituo hicho “Tumeona vituo vingine vinajengwa lakini vinafanya kazi nusu. Tunahitaji kituo chenye madaktari, wauguzi na dawa muda wote,” alisema mkazi mmoja aliyekataa kutajwa jina.

Mtaalamu wa maendeleo ya jamii, Mohammed Ibrahim, amesema changamoto za huduma za afya katika jamii za visiwani kama Tumbatu huchangia kuongezeka kwa vifo vinavyoweza kuzuilika, gharama kubwa za matibabu na mzigo wa kiuchumi kwa familia masikini.

“Ujenzi wa Kituo cha Afya Tumbatu ni hatua ya msingi katika kurejesha usawa wa huduma za afya kwa wananchi wa visiwani na kuchochea maendeleo ya kijamii,” alisema.

Serikali Yafafanua Mkakati wa Mradi

Akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, amesema kukamilika kwa kituo hicho kutaongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma za afya za msingi, ikiwemo huduma za mama na mtoto, huduma za dharura, maabara, kinga na tiba.

Amesema ujenzi wa kituo hicho ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya, hasa katika maeneo ya visiwani, ili wananchi wapate huduma kwa ukaribu na kwa viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali imeelekeza Wizara ya Afya kuhakikisha upatikanaji wa wataalamu wa kutosha, dawa, pamoja na gari la wagonjwa (ambulance) na huduma za dharura kwa saa 24.

Takwimu za Mradi na Uwajibikaji

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Mngereza Mzee Miraji, Kituo cha Afya Tumbatu kitakapokamilika kitahudumia zaidi ya watu 18,366 kutoka Tumbatu na maeneo ya jirani, kitaweza kulaza wagonjwa zaidi ya 30 kwa wakati mmoja na kutoa huduma za afya kwa saa 24, ikiwemo OPD, maabara, huduma za mama na mtoto na upasuaji mdogo na huduma za dharura .

Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Kisiwa cha Tumbatu kina wakazi 4,935, wakiwemo wanaume 2,302 na wanawake 2,633.

Mradi huo unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 6.4 za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, chini ya mkandarasi Simba Developer Ltd, na unasimamiwa na Idara ya Health Care Engineering and Infrastructure, huku ukitarajiwa kukamilika mwezi Machi 2026.

Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Kituo cha Afya Tumbatu umefungua ukurasa mpya wa matumaini kwa wananchi wa kisiwa hicho, lakini pia umeweka kipimo cha uwajibikaji kwa Serikali kuhakikisha kuwa ahadi zilizotolewa zinatafsiriwa katika huduma bora, endelevu na zenye tija.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *