WASICHANA ZANZIBAR WAJIKITA KATIKA MATUMIZI YA P2 ILI KUJILINDA NA UJAUZITO

“SIKU YA MTOTO WA KIKE DUNIA “

Na Abdul Sakaza

Ulimwengu leo unaadhimisha siku ya mtoto wa kike Duniani Siku ambayo huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 11,Umoja wa Mataifa leo unaadhimisha Siku hii ya Kimataifa ya Msichana 2025 kwa kaulimbiu “Mimi Mtoto wa Kike, Na Mabadiliko Ninayoongoza: Wasichana Katika kitovu cha Migogoro”, ikionesha jukumu la wanandoa kama wadau wa mabadiliko katika jamii zinazokumbwa na migogoro, majanga ya tabianchi, na wakimbizi.

Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa nchi zinazoadhimisha siku hii ya kimataifa ya mtoto wa kike siku hii tunaitazama kwa kuangalia kuongezeka kwa matumizi ya P2 miongoni mwa wasichana wadogo visiwani Zanzibar inaashiria wazi changamoto katika utekelezaji wa haki hizo, hasa katika elimu ya afya ya uzazi.

Elimu sahihi ya afya ya uzazi, mawasiliano mazuri kati ya wazazi na watoto, na usimamizi thabiti wa serikali juu ya uuzaji wa dawa hizi, ni hatua muhimu katika kulinda afya na mustakabali wa mtoto wa kike wa Zanzibar.Kitaalamu hujulikana kama ‘Emmergency Contraceptive Pills’ ni vidonge maalum vinavyotengenezwa kwa lengo la kutumika kwa dharura kuzuwia mimba isiyotarajiwa.

Zanzibar, kisiwa kinachojulikana kwa historia yake, utamaduni wake na mila zinazoheshimika, sasa kinakabiliwa na changamoto mpya ya kijamii na kiafya ya ongezeko la matumizi ya dawa za dharura za kuzuia mimba maarufu kama P2 miongoni mwa wasichana wadogo na wasioolewa.

Mara nyingi daktari huwandikia watu ambao wanashaka wa kupata ujauzito usiotarajiwa baada ya tendo kwa mfano ikiwa amebakwa na inatakiwa kutumika ndani ya saa 48 hadi 72 kupata matokeo. Kutumika kwa njia hii hakumzuii mtumiaji kutokupata magonjwa ya zinaaWataalamu wa afya wanasisitiza tembe hizo hazipaswi kumezwa mara kwa mara kwani vichocheo vilivyotumika kuitengeneza huweza kuathiri mwili wa mtumiaji.

Kupitia mahojiano na baadhi ya watumiaji wa p2 katika maeneo mbalimbali ya Unguja  imebainika kuwa idadi kubwa ya watumiaji wa dawa hizo ni wasichana wenye umri kati ya miaka 17 na 25, wengi wao wakiwa bado wanaishi chini ya ulizi wa  wazazi wao na wengine katika mazingira ya masomo.

Ni njia wanayoitazama kuwa rahisi na salama zaidi kwao katika kujilinda kutopata ujauzito  lakini matumizi yaliokithiri ya vidonde vya kuzuwia mimba kwa wasichana wengi inaweza kuwa hatari kwa afya zao, watalaam wanaonya.

Amina  singano miaka 22 mkaazi wa nungwi anasema yeye anatumia p2 kwa miaka mitatu sasa na imempa matokeo mazuri kwani kipindi chote hicho hajapata ujauzito na bado anaendelea kuzitumia “niliaza kutumia p2 wakati tulipopewa elimu ya  afya ya uzazi wakati nipo  chuo na sasa imenisaidia sana “alisema amina singano.

Neema ambae sio jina lake halisi miaka 18 mkaazi wa kiwengwa anasema aliaza kutumia p2 baada ya kushawishiwa na mpenzi wake ili  kujikinga na ujauzito kwani katika familia yake ujauzito ni aibu lakini anasema badae dawa hizo zilimsababishia maumivu ya tumbo na ada isiyotabirika “wezangu walikua na matokeo mazuri sana katika kutumia dawa hizi ila mimi nahisi hazinipendi” alisema Katika hali ya kushangaza.

si tu wanawake wanaotafuta matumizi ya p2 hata wavulana  huwanunulia wasichana wao dawa hizi kwa kile kinachojulikana njia ya kujikinga na  ujauzito”Mimi sijawahi kununua p2 lakini mweza wangu huniletea na hununua duka la dawa mkwajuni alisema Msichana huyu kutoka Mkokotoni kwa sharti la kutotajwa jina.

Monica miaka 20 mkaazi wa miembeni Unguja Anasema amekuwa akitumia tembe hizo mfululizo kwa kipindi cha miaka mitatu sasa ikiwa ndiyo mbinu yake kuu ya kudhibiti ujauzito baada ya kupokea habari kutoka kwa dada yake kuwa hakuna haja ya kutumia njia za uzazi wa mpango kuepuka mimba zisizotarajiwa.

Anasema dawa za p2   kwake anaona ni rahisi mno kupatikana katika maduka ya dawa tofauti na njia nyingine za kwenda kituo cha afya. “Niliamua mwenyewe kutumia, zinasaidia huwezi kupata mimba za usioihitaji na  zisizotarajiwa kwa sababu niseme ukweli nilianza mahusiano nikiwa bado mwanafunzi,” alisema

Asia kutoka jambiani anasema aliaza kutumia p2 akiwa chuo na Anasimulia kwamba tembe hizo huzinunua kwenye maduka ya dawa kwa kiasi cha Tsh. 3000 fedha ambayo hupatiwa na mweza wake .

Sio tu p2 imeleta mafanikio kwa watumiaji wapo ambao imewaathiri hadi leo na bado wanahangaika nayo kama anavyosimulia msichana huyu asietaka kutajwa jina lake miaka 19 mkaazi wa kitope Unguja “niliaza kutumia p2 tangu nipo darasa la tisa(kidato cha kwaza) wakati nna miaka 16 lakini sasa naugulia maumivu ya tumbo mwazo mama alisema chango ila nilipopata ada ya wiki 3 mfululizo madaktari wa hospital ya wilaya kivunge waliniambia nilipata madhara ya matumizi ya kupitiliza ya  p2 kwa muda mrefu “alisema

Kando na hilo pia  mazungumzo na wasichana kadhaa, imebainika kuwa wanaume wanaoshiriki nao katika mahusiano ya kimapenzi mara nyingi huwapa ushawishi au shinikizo la kutumia P2 badala ya njia nyengine “Mpenzi wangu hakubali kutumia njia yeyote ile Kila mara akiniahidi atanunua P2 baada ya tendo. Nimejikuta nikiitumia mara nne ndani ya miezi mitatu,” anasema Khadija miaka 23 mkazi wa Fuoni.

Wataalamu wa kijamii wanasema hali hii inaonyesha uhusiano usio sawa wa maamuzi ya afya ya uzazi baina ya wanaume na wanawake, Wanaume wanaonekana kushindikiza njia zinazowaacha wao bila majukumu, huku mzigo wa kiafya na kisaikolojia ukiwaangukia wasichana.

Nilizungumza na baadhi Wauzaji wa maduka ya dawa baridi yasiyopungua sita , mawili yakiwa katika Mkoa wa kaskaIzini unguja moja Mkoa wa kusini unguja na Matatu mkoa mjini magharibi, Wanasema njia hii ni rahisi na hata wasichana inawawia rahisi kuficha vidonge hivyo.

Wanasema vidonge hivyo wanaviuza mno kwa wasichana wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 25, rika ambalo wengi kati yao wapo kwenye mikono ya wazazi na walezi na bado wapo kwenye mfumo rasmi wa elimu.”Huwa tunawauliza kwanini wanajiingiza kwenye matumizi ya tembe hizi, wengi huwa hawataki kujieleza na wakati mwingine huja wavulana kuchukua badala ya wasichana, zinauzika sana,” anasema mmoja wa wauzaji  kutoka Mkoa wa Kusini Unguja ambaye hakupenda jina lake liwekwe hadharani.

Kadhallika Muuzaji mwengine kutoka duka la dawa mkoa wakaskazini unguja anakiri kua “ni kweli dawa hizi zinahitaji cheti cha daktari lakini tunawaonea huruma na sisi tunataka pesa, tena wananunua zaidi ya dozi moja, tunawauzia.

Alawi ambae sio jina lake haslisi yeye anasema kwa miaka ishirini sasa amekua akiuza dawa katika duka lake lililopo mjini Unguja anasema kwa miaka ya hivi karibuni dawa aina ya p2 ni miongoni mwa dawa maarufu zinazotoka kwa haraka ” zamani dawa za mafua ,homa na kifua zilikua zikitoka sana ila sasa p2 ndio zinazotoka sana kuliko dawa zozote dukani kwangu ” alisema

Kwa upande wao, wazazi wengi wameeleza masikitiko yao na  hofu kubwa juu ya mwenendo huu wa vijana kutumia dawa za p2 ili kujikinga na ujauzito na kuongeza kua matumizi ya P2 kwa wasichana wadogo yanaashiria pengo kubwa la mawasiliano baina ya wazazi na watoto wao nyumbani “Ni lazima wazazi tubadilike, tuzungumze na watoto wetu kabla hawajaangukia kwenye madhara,” anasema Bi Asha Omar, miaka 50 , mzazi wa watoto sita  mkazi wa Kidongochekundu.

Bi fatuma Ali Ameir mika 45 kutoka makunduchi ameeleza masikitiko yake kwa  vijana kuacha utamaduni wao na kuiga utamaduni wa kigeni wa kutumia dawa ili kujilinda na aibu ya mimba ” utashangaaa kwa nini watoto wetu wakiolewa wanakutwa sio wazima na kwanini hua kama wanafanya hivi vitendo wasipate mimba kumbe wanatumia dawa za p2 kwa kweli ni aibu” alisema bii fatma kwa uchungu.

Mzee Haji khamisi haji miaka 60 mkaazi wa muwange kaskazini Unguja anasema vijana wengi  sasa wanafahamu njia mballi mbali za kujikinga na ujauzito kutokana  na utandawazi wakati katika miaka iliopita hayakuwepo .”Haya mambo ya P2 si mazuri. Vijana wanakimbilia njia za mkato kwa sababu hawapati mwongozo. Serikali ifanye haraka kudhibiti, lakini na sisi wazazi pia tushiriki kuwafundisha watoto maadili na namna ya kujilinda” alisema mzee haji

YAFAHAMU MADHARA YA MATUMIZI YA P2

Kulingana na maelezo ya madaktari wa afya ya uzazi, P2 ni dawa ya dharura inayotakiwa kutumika mara chache, si zaidi ya mara moja kwa mzunguko wa hedhi, Matumizi ya mara kwa mara yanaweza kuleta madhara makubwa kama vile Kuvurugika kwa mzunguko wa hedhi,Kutokwa na damu isiyo ya kawaida,Kuongezeka kwa hatari ya kupata saratani ya kizazi endapo hutumiwa vibaya kwa muda mrefu na Madhara ya kisaikolojia yakiwemo wasiwasi na hofu ya kudumu.

Daktari Ummulkuruthum Omari Hamad ni  daktari bingwa wa afya ya uzazi katika Hospitali ya Mnazi Mmoja anasema “Kibaya zaidi ni kwamba baadhi ya wasichana huchukulia P2 kama njia ya kawaida ya uzazi wa mpango. Hii ni hatari sana kwa sababu inaweza kuharibu kabisa mfumo wao wa uzazi na hata kupelekea utasa.”

Ameongeza kua p2 zinatakiwa kutumiwa kwa maelekezo ya Daktari na kwa lengo lililokusudiwa na si vyenginevyo kwani kinyume na hivyo p2 inaweza kuleta madhara ya muda mrefu ikiwemo saratani ya mlango wa shingo ya kizazi .

Pia Kwa mujibu wa national Cancer lnstitute kutoka marekani kutumia vidonge vya kuzuia mimba kunaweza kuongeza hatari ya kupata saratani hususan ni ya matiti ,ovari na shingo ya kizazi

Je, Wizara ya Afya Zanzibar inataambua changamoto hii ? na itachukua mikakati gani  ya kudhibiti matumizi holela ya P2 kwa wasichana hapa visiwani Zanzibar ni suala linalouliziwa na wengi na tulipotaka kufahamu hili kutoka kwa vizara husika ya afya  wiki mbili mfululizo jitihada za kupata ufafanuzi ziligonga mwamba .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *