Na Abdul Sakaza
Kanisa Katoliki Zanzibar limevihimiza vyombo vya habari visiwani hapa kuongeza kasi ya kuripoti habari zinazohusu haki za binadamu na utawala bora ili kusaidia kupunguza migogoro na kuleta usawa katika jamii
Wito huo umetolewa na Sister Editha Asiimwe, ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Kanisa Katoliki Zanzibar, wakati wa ufunguzi wa mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Utengemano Welezo (Peace Building Center).

Sister Asiimwe amesema kuwa lengo kuu la mradi huo wa uwezeshaji jamii ni kuongeza uelewa kuhusu haki za binadamu na misingi ya utawala bora, huku ukigusa pia kusaidia watu wenye ulemavu, wanawake, na vijana kiuchumi. Aidha, amebainisha kuwa mradi huo unatazama pia mahitaji ya watoto wenye mahitaji maalum ili kuhakikisha kunakuwepo na usawa wa kijamii katika maeneo yote.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Dokta Sikujua Omar amebainisha kuwa bado jamii haina mwamko wa kutosha wa kuripoti habari za udhalilishaji na matukio ya uvunjaji wa haki za binadamu,amesisitiza kuwa ni jukumu la vyombo vya habari kuripoti habari hizo kwa kina ili kuisaidia jamii kupaza sauti zao na kupata haki stahiki pale zinapokiukwa.

Kwa upande wake, Afisa wa Tathmini na Ufuatiliaji wa Idara ya Maendeleo Zanzibar, Msafiri Thomas Mombo, amesema kuwa mafunzo hayo yanalenga pia kuwawezesha wasaidizi wa sheria ili waweze kutoa elimu na usaidizi wa kisheria kuhusu masuala ya udhalilishaji na sheria kwa ujumla.
Mwanasheria wa mradi huo, Peter Maswi Marwa, ameongeza kuwa vyombo vya habari vina nafasi ya kipekee ya kutoa elimu ya sheria na haki za binadamu kwa watu wengi kwa wakati mmoja kwaji kufanya hivyo itaisadia jamii kupata uelewa wa kutosha juu sheria hizo

Nao waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo wameahidi kuendelea kuripoti habari hizo kwa weledi ili kusaidia kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.
Mradi huo unatarajia kuwahusisha wasaidizi wa sheria, viongozi wa dini, pamoja na viongozi wa shehia ili 1kufikia malengo yaliyokusudiwa ya kuleta utulivu na haki visiwani Zanzibar.
