“KALAMU NA HARAKATI ZIWE SILAHA YA MABADILIKO KATIKA JAMII YENU” Waandishi Wa Habari Na Wadau Waaswa Zanzibar

Na Abdul Sakaza

Akiipoti Kutoka Zanzibar

Imeboshwa Saa 9 Zilizopita

Katika hali inayozidi kuonyesha umuhimu wa vyombo vya habari na asasi za kiraia katika maendeleo ya taifa, wadau wa sekta hizo visiwani Zanzibar wametakiwa kuacha tabia ya kuripoti matukio kama simulizi na badala yake kuwa injini ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoididimiza jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari na viongozi wa Asasi za Kiraia katika mafunzo ya siku mbili yalioandaliwa na taasisi ya Pamoja Youth Initiative (PYI) ambayo yalifanyika katikaukumbi wa mikutano wa Skuli ya Tumekuja, Kijangwani Zanzibar, Mratibu wa Mtandao wa Haki za Binadamu Zanzibar (THRDC), Suleiman Muyuni Baitani, amesema waandishi wa habari na viongozi wa Asasi za Kiraia wana nafasi kubwa ya kuibua matatizo yanayoikumba jamii na kusaidia kuyatafutia ufumbuzi.

“Sisi ni daraja. Ni jukumu letu kisheria na kimaadili kuibua changamoto zinazoikabili jamii yetu, hususan vijana, na kuhakikisha hatuishii tu kusema kuna tatizo, bali tunashirikiana na mamlaka husika kutafuta ufumbuzi wa kudumu,” alisisitiza Bw. Baitani.

Aliongeza kuwa ni vyema waandishi wa Habari wakajikita  katika kujifunza mbinu za kisasa za uandishi wa habari za kijamii (Social Impact Journalism) ili kuripoti hbari za kiraia (civil report) ambazo matokeo yake ni kuleta mabadiliko ya moja kwa moja kwa mwananchi.

Mussa Mbwara  ni Mkuu wa Utawala wa Pamoja Youth Initiative (PYI), aligusia kundi la vijana ambalo mara nyingi hukwama kutokana na ukosefu wa fursa, Alisema kuwa taasisi yake inatambua kiu ya vijana wengi ni  kupata mikopo na mitaji, na hapo ndipo mchango wa habari za kijamii unapohitajika kuchochea sera rafiki na kuibua fursa zilizojificha.

Kwa upande wake, Afisa Programu wa PYI, Daudi Kassim, alibainisha kuwa kikwazo kikubwa si upungufu wa matukio ya kijamii, bali ni uelewa mdogo wa namna ya kuyatambua na kuyafanyia kazi kwa weledi.

Afisa huyo alibainisha kua jambo muhimu kwa  waandishi na wanaharakati kuzingatia misingi ya sheria za nchi wanapotekeleza majukumu yao. “Unaporipoti tukio la kijamii, ni lazima uwe na vielelezo na uthibisho usiotia shaka. Huwezi kuleta mabadiliko kama taarifa zako hazina mashiko ya kisheria au kidokezo cha ukweli uliothibitika,” alisema.

Washiiki wa mafunzo hayo wakiwemo waandishi wa Habari na wadau wa asasi za kiraia wamesema mafunzo hayo yamewasaidia kuelewa namna bora ya kuripoti habari za kijamii na kushiriki katika kutatua mbali mbali za kuibua matatizo yanayowakumba wananchi

lengo la mafunzo hayo yalioandaliwa na taasisi ya Pamoja Youth Initiative (PYI) ni kuwaongezea uwezo waandishi wa habari na viongozi wa Asasi za Kiraia katika kuripoti matukio mbali mbali yanayoikumba jamii

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *