Na Abdul Sakaza,
Akiripoti kutoka Mkokotoni Kaskazini Unguja
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Vijana na Elimu Wilaya ya Kaskazini “A” (JUVIEKA), Mbarouk Maalum Mohamed, amewataka vijana kutumia vyema haki yao ya kupiga kura kwa kuchagua viongozi sahihi na kudumisha amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu .
.Akizungumza na Radio One, Sakaza Digital Blog na Tumbatu FM wakati wa utoaji wa elimu ya mpiga kura katika ofisi za JUVIEKA zilizopo Mkokotoni, Mbarouk alisema ni muhimu kwa vijana kutokubali kutumiwa kama chombo cha kisiasa, bali wawe chachu ya kuimarisha umoja na mshikamano katika jamii.
“Vijana tunapaswa kuelewa kuwa sauti yetu kwenye kura ina nguvu kubwa. Tusikubali kutumiwa kwa maslahi binafsi ya wanasiasa, bali tuweke mbele mustakabali wa nchi yetu,” alisema Mbarouk.
Aidha, aliwasisitiza vijana na wananchi kwa ujumla kutunza amani kwa gharama yoyote, akisema amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo ya taifa. “Uchaguzi unakuja na unaisha, lakini amani inatakiwa ibaki daima. Bila amani hakuna maendeleo, hakuna elimu bora, wala uchumi imara,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Mbarouk aliwahimiza vijana kuwa wazalendo na kufikiri kwa upana kuhusu maisha baada ya uchaguzi, akieleza kuwa kuendeleza chuki za kisiasa hakusaidii katika kujenga taifa lenye umoja. “Kura yako ni siri yako, ila matokeo yake ni mustakabali wa nchi nzima. Tuwe wazalendo, tupende nchi yetu na tujitahidi kuchangia maendeleo kwa njia chanya,” alisema.

Kwa upande mwingine, Mbarouk amewashauri wanasiasa kuweka mbele maslahi ya taifa badala ya maslahi binafsi, akibainisha kuwa nafasi za uongozi ni dhamana, si fursa ya kujinufaisha.> “Ni wajibu wa kila mwanasiasa kutanguliza maslahi ya taifa. Wananchi wanahitaji maendeleo, si migogoro wala maneno ya uchochezi,” alisisitiza.
Kampeni hiyo ya elimu ya mpiga kura inaendelea katika shehia mbalimbali za Wilaya ya Kaskazini “A”, ikiwa na lengo la kuwajengea vijana uelewa juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi kwa amani na kuwajibika kidemokrasia.
