NA FAUZIA MUSSA
JUMUIYA ya Uhifadhi Mji Mkongwe (JUHIMKO) imeiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuendeleza ushirikiano katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, ambazo zimeendelea kuathiri maeneo mbalimbali ya Zanzibar, hususan Mji Mkongwe ambao ni urithi wa dunia uliotambuliwa na UNESCO.
Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa ziara maalum ya kutembelea maeneo yaliyoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi, Ofisa Mtendaji wa JUHIMKO, Makame Juma Mtwana, alisema juhudi za pamoja kati ya Serikali, jamii na wadau ni muhimu kwa ajili ya kulinda historia na utajiri wa kiutamaduni wa Mji huo.
Aidha aliziomba Serikali zote kushrikiana Katika kujenga ukuta wa ulinzi ualioanzia forodhani Hadi malindi Ili kuzuia athari za mabadiliko ya tabia Nchi zinazotishia mustakabali wa Mjihuo. “Tunaomba Serikali imalizie ujenzi wa ukuta kutoka Forodhani hadi Malindi ili kuhifadhi maeneo hayo. Mji Mkongwe ni urithi wa dunia na mchango wake katika kukuza utalii na uchumi wa Zanzibar ni mkubwa,” alisema Mtwana.

Alisema kujengwa Kuta pembezoni mwa bahari ya mji huo kutasaidia Kwa kiasi kikubwa kupunguza athari za kimazingira na kuuwacha mji mkongwe ukiwa salama na kuendelea na hadhi yake ya urithi wa dunia.Alifafanua kuwa mabadiliko ya tabia nchi si tatizo la Zanzibar pekee, bali ni changamoto ya kidunia.
Hivyo, ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, jamii na mashirika ya kiraia kama JUHIMKO ni muhimu sana katika kulinda mazingira na kuhifadhi historia ya visiwa vya Zanzibar kwa sasa na vizazi vijavyo.
Aliongeza kuwa JUHIMKO itaendelea kutoa elimu kwa jamii ili kuiwezesha kuelewa athari za kimazingira zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi na namna ya kuzizuia, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali Katika kukabiliana na hali hiyo.
Mapema aliwahimiza waandishi wa habari kuwa mabalozi wa mabadiliko ya tabia nchi kwa kutoa taarifa na kuhamasisha jamii kushiriki katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.

Kwa mujibu wa Othman Bakar Burhan kutoka Idara ya Mazingira, kitengo cha mabadiliko ya tabia nchi, maeneo 145 yameathiriwa moja kwa moja na mabadiliko ya tabia nchi yakiwemo 25 Unguja na 143 Pemba.“Fukwe, makazi na miundombinu ya barabara yote yameathiriwa. Serikali inaendelea kuchukua hatua za kurejesha maeneo haya katika uasili wake,” alisema Othman.
Othman alizitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na kupanda miti, kujenga matuta na kuta za mawe kando ya bahari.” Kwa mfano, mwaka 2017, hekta nne za mikoko zilipandwa na kuta nane za mawe kujengwa katika fukwe ya Kilimani kwa lengo la kudhibiti maji ya bahari yasiingie kwenye makazi.” Alisema Othman.
Aidha, alieleza kuwa Serikali imeanzisha Mamlaka ya Mazingira yenye kitengo maalum cha mabadiliko ya tabia nchi chenye jukumu la kutoa elimu kwa jamii kuhusu athari za mazingira na namna ya kukabiliana nazo kama hatua na sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Kwa Upande wake Mohamed Ibrahim Jidawi, Mwenyekiti wa Kamati ya Usafi na Mazingira Shehia ya Malindi, alisema kuwa asilimia 75 ya athari za mazingira zinachangiwa na tabia za kibinadamu.“Fukwe ziligeuzwa kuwa dampo kwa zaidi ya miaka 10, hali iliyosababisha taka kusukumwa hadi kwenye makazi ya watu na kuhatarisha afya zao,” alieleza Jidawi.
Abdalla Saidi Abdalla (51), Mwenyekiti wa Hifadhi ya Changuu Bawe (CHABAMKA), alibainisha kuwa fukwe ya Betras zamani ilikuwa ikitumika kwa michezo na shughuli nyingine, lakini kwa sasa haiwezi kutumika tena kutokana na athari za kimazingira.“Baadhi ya wavuvi hutumbukiza mchanga baharini kwa ajili ya uvuvi, jambo linaloharibu mazingira ya bahari na kuchangia kina cha maji kupanda. Tunataka kuanzisha sheria itakayowabana wanaofanya vitendo hivi,” alisema Abdalla ambae NI mzaliwa wa eneo la Sharifmsa Sheha wa Sharifmsa.

Wanu Makame Hassan, alisisitiza kuwa bado kuna uhitaji mkubwa wa elimu kwa jamii kuhusu athari za mabadiliko ya tabia nchi na kutoa wito kwa idara husika kushuka kwa wananchi na kujenga uelewa wa pamoja ili kuleta mafanikio ya kudumu katika vita dhidi ya mabadiliko hayo.
Ziara hiyo iliyowakutanisha waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari ambao walitembelea katika maeneo ya Betras, Chuini, Malindi na Kilimani Chini, ambapo athari za mabadiliko ya tabia nchi zimeonekana wazi. Maeneo hayo yameshuhudia mmomonyoko wa fukwe, maji ya bahari kuingia kwenye makazi ya watu na maeneo ya kilimo.
