HAKIKISHENI WATOTO HAMUWACHUKUI KATIKA MIKUTANO YA KAMPENI ZA KISIASA WAZAZI ZANZIBAR WATOA NENO

Na Samira Ali.

Follow up of the Story: Abdul Sakaza

Katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, wazazi na walezi wametakiwa kuacha tabia ya kuwachukua watoto kwenye mikutano ya kampeni za kisiasa.

Taasisi za kijamii na za wanawake Zanzibar zimeonya kuwa kitendo hicho kinaweka watoto katika mazingira hatarishi kiafya na kiusalama, huku kikinyima haki yao ya malezi bora.

Taasisi hizo ni pamoja na JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA, na TAMWA-ZNZ, ambazo kwa kushirikiana na Ubalozi wa Norway, zimeeleza kuwa mikutano ya kisiasa mara nyingi huhusisha msongamano, kelele na matendo yasiyofaa kwa watoto.

Wameeleza kuwa watoto sio wapiga kura na uwepo wao kwenye mikutano hiyo hauna faida, bali huongeza hatari ya kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili.

Aidha taasisi hizo zimeeleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Zanzibar Na. 6 ya 2011, kifungu cha 14(1) kinatamka wazi kuwa mtoto anatakiwa kulindwa dhidi ya mazingira yanayoweza kuhatarisha maisha au afya yake.

Vilevile, Tanzania imeridhia mikataba ya kimataifa na kikanda ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Watoto (CRC) na Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (ACRWC) ambayo inasisitiza ulinzi na ustawi wa watoto.

Takwimu kutoka Afisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali (OCGS) zinaonyesha kuongezeka kwa matukio ya ukatili na udhalilishaji dhidi ya watoto kila mwezi ambapo kwa mwezi wa Juni 2025 kulikuwa na  matukio 97, ambapo matukio  83 sawa na asilimia (85.6%) walikuwa watoto, pia kwa mwezi wa Julai 2025 Matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yalikuwa 107, ambapo waathirika watoto walikuwa  95 sawa na asilimia (88.8%) na kwa mwezi Agosti 2025 Matukio hayo yalikuwa 116,na waathirika  watoto ni 104 (89.7%).

kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA-ZNZ wamewataka viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini, wazazi, walezi na vyombo vya habari kushirikiana katika kutoa elimu na kuchukua hatua za kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili.

MAONI YA WANANCHI

Baadhi ya wananchi pia wameeleza mtazamo wao kuhusu tatizo hilo, wakisisitiza kuwa wazazi wanapaswa kubeba jukumu la kulinda usalama wa watoto.

Mariam Ali, mkazi wa Fuoni mwenye umri wa miaka 34, amesema kuwa mara nyingi ameshuhudia wazazi wakihangaika na watoto wadogo kwenye mikutano ya kisiasa, jambo linalowaweka hatarini hasa pale kunapotokea vurugu.“Watoto ni wadogo, hawawezi kujilinda. Wazazi tunapaswa kubeba jukumu la kuhakikisha hawafiki katika maeneo hayo yenye msongamano mkubwa,” alisema Mariam.

Juma Khamis, kijana wa miaka 27 kutoka Kitope, ameeleza kuwa tatizo hili mara nyingi huzingatiwa kidogo, huku wazazi wengine wakiona kama ni jambo la kawaida.“Kumchukua mtoto kwenye mkutano wa kisiasa si kumsaidia bali ni kumuweka katika mazingira ya hatari. Ni bora wabaki nyumbani wakiwa salama,” alisema Juma.

Fatma Omar, mama mwenye umri wa miaka 41 kutoka Mkokotoni, amesema kuwa ni jukumu la viongozi wa kisiasa pia kuelimisha wafuasi wao kuhusu hatari za kuwaleta watoto kwenye kampeni. “Nafikiri viongozi wa kisiasa pia wanapaswa kusema wazi kuwa hawataki kuona watoto katika mikutano yao. Hapo wazazi watachukua tahadhari zaidi,” alisema Fatma.

Moh’d Khamisi ni kijana kutoka shehia ya Mto wa pwani anasema Watoto wana haki ya kukua katika mazingira yenye amani, kucheza, kujifunza na kufurahia maisha ya utoto bila kubebeshwa mizigo ya itikadi au mashinikizo ya kisiasa.”Watoto ni hazina ya kesho. Tuwape nafasi ya kukua wakiwa salama, huru, na wasiofungwa na misimamo ya kisiasa. Tuwalinde leo ili walinde taifa kesho” alisema Moh’d

Kwa pamoja, JUWAUZA, PEGAO, ZAFELA na TAMWA-ZNZ wamesisitiza kuwa viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini, wazazi, walezi na vyombo vya habari wanapaswa kushirikiana katika kutoa elimu na kuchukua hatua madhubuti za kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na ukatili, hasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *