
Na Faudhia Abdallah -Zanzibar
MKUU wa Wilaya ya Magharibi ‘A’, Cassian Gallos Nyimbo, ameonesha msimamo thabiti dhidi ya uvamizi na uharibifu wa ardhi ya kilimo, baada ya kutangaza rasmi kulitaifisha eneo la kilimo lililoko Shehia ya Mwakaje Saraya, kufuatia hatua za kinyume cha sheria za kuuza na kuanzisha ujenzi kiholela.
Eneo hilo linalodaiwa kuwa mali ya Moh’d Faridi Seif, limeuzwa kwa mtu mmoja aitwaye Moh’d Shaibu Salmini bila kufuata utaratibu wa kisheria wa kuhamisha matumizi kutoka kilimo kwenda makazi.
Alisema mauzo hayo yalikadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 300, yameambatana na uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwa ni pamoja na kukatwa kwa miti mingi na zaidi ya minazi 120.
“Eneo hili halikupaswa kuguswa kabla ya kufikishwa kwenye Mamlaka ya Ardhi na Upimaji kwa ajili ya mchakato wa mabadiliko ya matumizi. Hatuwezi kuruhusu mtu kuchukua sheria mkononi na kuligawa kiholela. Hatua zimechukuliwa, na zitaendelea kuchukuliwa,” alisema DC Nyimbo.
Aidha aliongeza kuwa hakuna atakayevumiliwa endapo atakwenda kinyume na taratibu za matumizi ya ardhi,alibainisha kuwa tayari mtuhumiwaamekamatwa na atafikishwa mahakamani, huku akisisitiza kuwa haki itatendeka kwa mujibu wa sheria.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Magharibi ‘A’, Moh’d Simba Hassan, alieleza kuwa ofisi yake haijawahi kupokea taarifa zozote kuhusu uuzaji wa ardhi hiyo wala kutoa kibali cha ujenzi katika eneo hilo.
“Katika uongozi wangu, sitakubali uharamia wa aina hii. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote wanaohusika,” alisema Simba kwa ukali.
Naibu Katibu Mtendaji kutoka Kamisheni ya Ardhi, Mussa Kombo, alikazia kuwa ni kosa kisheria kubadilisha matumizi ya ardhi bila idhini ya kamisheni.
“Hatutarajii kuona watu wakiharibu ardhi ya kilimo, wakati dunia inapambana na changamoto ya uhaba wa chakula,” alionya.
Hali hiyo pia imezua sintofahamu kwa Sheha wa Mwakaje Saraya, Kasongo Moh’d Kasongo, ambaye alidai kutokuwa na taarifa yoyote rasmi kuhusu uuzaji huo, akieleza kuwa wahusika hawakuwahi kufika ofisini kwake kwa maelezo au kibali.
Kwa upande wa muuzaji wa shamba hilo amedai ni mali ya kurithi kutoka kwa marehemu baba yao, huku mnunuzi akithibitisha kuwa alilinunua kwa makubaliano halali na alianza kuligawa kwa matumizi ya makazi.
Tukio hili limeibua mjadala mpana kuhusu usalama wa ardhi ya kilimo visiwani Zanzibar, na kuzifanya mamlaka husikakuhamasisha utunzaji wa ardhi kwa kuzingatia sheria na mazingira.
