NA MAUA ABDALLA BMMA
Baraza la Manispaa Magharibi “A” limeendesha zoezi la kuvunja vibanda vya wafanyabiashara wadogowadogo waliokuwa wakiendesha shughuli zao pembezoni mwa barabara katika eneo la Chuini, Wilaya ya Magharibi “A”.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalum za SMZ, Mheshimiwa Masoud Ali Mohamed, aliyelitoa baada ya kufanya ziara ya ukaguzi katika soko jipya la kisasa lililojengwa kwa ajili ya wafanyabiashara wa eneo hilo na maeneo jirani.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Waziri alijiridhisha na hali ya usafi, uimara wa miundombinu na mazingira bora yaliyopo sokoni hapo, na kueleza kuwa soko hilo sasa liko tayari kwa matumizi.
Aidha, alitangaza kuwa ufunguzi rasmi wa soko hilo unatarajiwa kufanyika tarehe 4 Agosti 2025, ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi.
Na katika muktadha huo ndipo Waziri Masoud alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Magharibi “A”, Moh’d Simba Hassan, kuwaondoa wafanyabiashara wote waliokuwa wakifanya biashara pembezoni mwa barabara na kuwaelekeza kuhamia kwenye soko hilo jipya la kisasa.

Akizungumzia utekelezaji wa agizo hilo, Mkurugenzi Simba alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imejipanga kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya shughuli zao katika mazingira rafiki, yenye usalama na miundombinu bora ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi.“Vibanda vilivyokuwa vimejengwa kiholela kandokando ya barabara vilikuwa havina sifa za kiusalama, vinaharibu mandhari ya mji, na kuhatarisha maisha ya wafanyabiashara pamoja na wateja wao. Tunawahimiza wahusika wote wahamie sokoni kwa ajili ya maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla,” alifafanua.
Aidha, Mkurugenzi alitoa wito kwa wafanyabiashara wote kushirikiana na Serikali katika kutunza mazingira ya soko jipya, kuhakikisha usafi na kutumia miundombinu iliyopo kwa ufanisi.Zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara kutoka maeneo yasiyo rasmi limepokelewa kwa hisia tofauti na baadhi ya wahusika, ambapo baadhi yao wameomba kuendelea kushirikishwa mapema kabla ya utekelezaji wa hatua kama hizo ili kuepusha usumbufu na madhara ya kiuchumi.

Hata hivyo, Serikali imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza ujenzi wa masoko ya kisasa visiwani Zanzibar kama sehemu ya mpango wa kuwawezesha wananchi kiuchumi na kuboresha hadhi ya miji na kuongeza mapato ya taifa kwa ujumla.
